Description
Bwana Yesu Asifiwe sana mpendwa wetu katika Kristo! Awali ya yote tunamshukuru Bwana Yesu Kristo kwa kutupatia neema ya kuona mwaka mwingine 2024. Hivyo basi tunatumia pia fursa hii kukutakia wewe na familia yako heri na fanaka ya Mwaka Mpya 2024.
Mwongozo huu ni kwa ajili ya maombi ya kuanza Mwaka 2024 na kuomba baraka na mafanikio ya KIMUNGU kwenye kipindi chote cha mwaka mzima.
Mwaka mpya ni msimu mpya na hivyo kuna namna na wewe unaingia msimu mpya. Acha nikuambie jambo muhimu kuhusu msimu. Dunia huzunguka jua kwa siku 365 na tunapata majira mbali mbali ya hali ya hewa ama vipindi mbali mbali kutokana na Dunia kuzunguka jua. Vivyo hivyo katika ulimwengu wa roho tunazunguka jua la uzima ambaye ni Bwana Yesu na tunapata majira mbali mbali. Malaki 4:2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza- cheza kama ndama wa mazizini.
Katika kuzunguka huwa kuna vipindi au majira ya tofauti tofauti katika ulimwengu wa roho, hivyo vipindi au majira ni vya muhimu sana kwa kuwa kila kipindi kina jambo la rohoni.
Mhubiri 3:1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
Kwenye ulimwengu wa roho, msimu mpya ni mafunuo na neno la Mungu ambalo mtu akitii anaweza kuingia kwenye msimu mpya katika maisha yake kiroho. Mfano, mtu anaweza kuingia kwenye kipindi cha baraka na mafanikio ya kipekee sana akitii neno la msimu na endapo atakuwa makini asipitwe na majira ya kujiliwa kwake. Ni muhimu sana kwako kutambua wakati, majira na kuwa na nia ya kuingia msimu mpya kwa kutegemea mkono wa Bwana kutenda kazi juu yako.
Reviews
There are no reviews yet.